Kamishna wa kaunti ya Nyamira Josphine Onunga amejitokeza kuwaonya vikali machifu na manaibu wao dhidi ya kujihusisha na masuala ya kisiasa.
Kwenye mahojiano kwa njia ya simu mapema Jumatatu, Onunga alisema kuwa maafisa wa umma hawastahili kujihusisha na masuala ya kisiasa huku akionya kuwa yeyote atakayepatikana atachukuliwa hatua kali.
"Maafisa wa umma hawaruhusiwi kujihusisha na masuala ya kisiasa, na ni onyo langu kwa machifu na manaibu wao wanaojihusisha na siasa, na kwa kweli yeyote atakayepatikana atachukuliwa hatua kali za kisheria," alisema Onunga.
Onunga aidha aliongeza kwa kuwahimiza machifu na manaibu wao kupambana na ugemaji na ubugiaji wa pombe haramu.
"Vita dhidi ya pombe haramu vingalipo na yeyote atakayepatikana akiendelesha biashara hiyo atachukuliwa hatua kali kwa mujibu wa sheria kwa maana tunataka kuwaokoa watu wetu kutokana na ubugiaji pombe haramu," aliongezea Onung'a.