Share news tips with us here at Hivisasa

Maafisa wa afya ya umma katika kaunti ndogo ya Nyamira wameomba ushirikiano wa washikadau mbalimbali ili kusaidia kuangamiza funza.

Akihutubu katika eneo la Kebirigo siku ya Jumatatu wakati wa uzinduzi rasmi wa kampeni ya siku nne yakuangamiza funza, afisa wa afya ya umma Fred Mogotu alisema kuwa visa vya kuathirika na funza vimekuwa vikiongezeka katika eneo hilo.

"Tumekuwa tukitia juhudi zakuhakikisha kuwa tunaangamiza funza katika Kaunti ya Nyamira lakini visa hivyo vinaendelea kuongezeka.

Kaunti ndogo ya Nyamira ina asilimia saba ya ongezeko la funza ikilinganishwa na asilimia tano kwenye kaunti nzima ya Nyamira,” alisema Mogotu.

Mogotu alisema ongezeko la funza husababishwa na uchafu na akisisitiza kuwa hali yakutojengwa vizuri kwa sakafu za shule pia huchangia pakubwa kusambaza funza hao.

Aliwahimiza wasimamizi wa shule mbalimbali kuhakikisha kuwa sakafu za shule zinaezekwa vizuri ili kudhibiti janga hilo la funza.

"Kulingana na utafiti tuliofanya, funza hawa huletwa na hali yakutozingatia usafi na kutoezekwa vizuri kwa sakafu hasa shuleni. Nawahimiza walimu wakuu kuhakikisha kuwa sakafu zimeezekwa vizuri ili kuepukana na funza," alisema Mogotu.

Afisa huyo wa afya ya umma aidha alisema kuwa idara ya afya ina mipango yakufanya misururu ya mikutano yakuwahamasisha washikadau mbalimbali ili washirikiane kikamilifu kuhakikisha kuwa viwango vya umaskini vimepungua ili kusaidia kudhibiti ongezeko la funza.

"Idara ya afya ina mipango yakufanya misiruru ya kampeni kote Nyamira ili kuwahimiza wananchi kutoka matabaka mbalimbali kushirikiana kuangamiza umaskini kama njia mojawapo yakupambana na funza," alisema Mogotu.