Kampeini ya chanjo dhidi ya ugonjwa wa kupooza yaani Polio, imeratibiwa kuanza Jumamosi huku wizara ya afya ikilenga watoto wapatao milioni 8.4.
Wizara hiyo imesema tayari kaunti zote 47 zimepewa faedha kufanikisha shughuli hiyo huku dawa zitakazotumika zikitarajiwa kuanza kusambazwa kwenye kaunti hizo kuanzia hii leo hadi siku ya Ijumaa.
Kaimu mkurugenzi mkuu wa huduma za matibabu, Jackson Kioko anawataka akina mama kushurutishwa kuonyesha kijitabu kinachodhihirisha kuwa wanao wamepata chanjo hiyo kabla ya kuruhusiwa kujiunga na shule ili kuwawezesha watoto wote kupata chanjo hiyo muhimu.
“Ni vipi ambavyo tunapaswa kuhakikisha kuwa akina mama wanathamini pakubwa kijitabu hiki kinachohakikisha kuwa wanao wanapokea matibabu yanayozuia magonjwa yoto hadi pale mwanawe anapojiunga shuleni? Hili linawezekana kuwalinda watoto wtu na kuwakinga kufuatia magonjwa ya kupooza,” alisema Kioko.
Aliongeza kuwa maafisa wa afya watazuru makanisani na misikitini ili kuwawezesha kuafikia idadi iliyowekwa.
Kampeini ya mwezi jana iliyoandaliwa kwa kaunti 13 ikiwemo West Pokot, Turkana, Marsabit, Mandera, Garissa, Wajir, Tana River, Lamu miongoni mwa kaunti nyinginjezo ilifaulu kuwapa chanjo zaidi ya watoto milioni moja kama ilivyokusudiwa.