Serikali ya Kaunti ya Mombasa hatimaye imezindua rasmi kampeni ya usafi katika shule za kaunti, itakayolenga kuimarisha mazingira bora miongoni mwa wanafunzi pamoja na jamii.
Kampeni hiyo iliyopewa jina “Mambo Safi” ilizinduliwa rasmi siku ya Jumamosi na gavana wa kaunti hiyo Hassan Joho, pamoja na mkuu wa idara ya mazingira Tendai Lewa.
Katika taarifa kwa vyombo vya habari, Gavana Joho alisema kuwa hivi karibuni wataanzisha shughuli ya kuhamasisha wanafunzi katika shule za eneo hilo jinsi ya kudhibiti uchafu na kuweka mazingira safi.
“Kupitia kwa kamati maalum ya mazingira katika kaunti, tutaanzisha huo mpango ikiwa ni pamoja na shughuli ya upanzi wa miti shuleni,” alisema Joho.
Takriban wanafunzi 30,000 kutoka shule mbalimbali katika kaunti hiyo wamehusishwa na kampeni hiyo ambayo inatarajiwa kuugeuza mji wa Mombasa kuwa moja kati ya miji safi zaidi hapa nchini.
Hapo awali, mkuu wa idara ya mazingira Tendai Lewa alieleza kwamba kutakuwa na programu maalum kila Jumamosi ya tatu ya kila mwezi ambapo shule zote zitakuwa zinahusika katika zoezi la usafi katika shule zao.
Hata hivyo, Gavana Joho aliongeza kwamba mpango huo sio tu kwa wakaazi wa Mombasa peke yake, bali pia maeneo jirani yatanufaika na mradi huo.
Kampeni hiyo inakuja huku kukiwa na shinikizo kutoka kwa washikadau katika sekta ya utalii wanaotaka serikali ya kaunti kuimarisha usafi wa mji ili kuvutia watalii wanapozuru mji huo.
Wadau hao walisema kuwa haileti picha nzuri wakati wageni kutoka mataifa ya mbali wanapozuru Mombasa, na kupata mji huo ukiwa mchafu, ilhali ni moja kati ya miji mikuu inayosifika kwa utalii duniani.