Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Jumla ya kampuni tano za kutengeneza maji ya chupa ya kunywa al maarfu 'mineral water' yamepigwa maruuku mjini Mombasa baada ya uchunguzi kuibaini kuwa maji hayo si safi kwa matumizi ya binadamu.

Akizungumza na wanahabari, Mkuu wa Idara ya Afya Kaunti ya Mombasa Mohamed Abdi alisema kuwa baadhi ya maji hayo yalipatikana na vidudu ambavyo vinaweza kusababisha maradhi ya kipindupindu.

Aidha, mkuu huyo wa idara alisema ameshangazwa kwa kuidhinishwa kwa kampuni hizo na shirika la udhibiti wa bidhaa nchini KEBS, licha ya kutoweza kuafikia kigezo hitajika.

Abdi amewataka wenye maduka yanayouza maji hayo kusitisha biashara hiyo kuondoa bidhaa hizo kwenye maduka yao kwani hivi karibuni wataanzisha msako wa maji hayo kwenye maduka yote.

Itakumbukwa kuwa Idara ya Afya Kaunti ya Mombasa ilitangaza kuzuka kwa maradhi ya homanyongo A amabayo yalisemekana kusababishwa na matumizi ya maji machafu.

Swala la usambazaji wa maji safi katika Kaunti ya Mombasa limekuwa changamoto kubwa kwa muda mrefu huku wengi wa wakaazi wakitegemea maji ya visima ambayo ni ya chumvi.

Kampuni zilizopigwa marufuku ni Bamba processed katika eneo la Nyali, Zahra Cool huko Ganjoni, Zeit (Kisauni), Active (Bombolulu), na Sundus katika eneo la Majengo.