Basi la kampuni ya Mombasa Raha.[Picha/ mombasarahabooking.com]
Kampuni ya mabasi ya Mombasa Raha inakadiria hasara ya takriban shilingi milioni 2.5 baada ya halmashauri ya uchukuzi na usalama wa barabarani NTSA, kusitisha huduma za mabasi hayo kwa takriban wiki moja sasa.
Amri hiyo ilitolewa kwa kampuni zote za magari zinazohudumu chini ya chama cha ushirika cha Star Ways Express Limted.
Akizungumza na waandishi wa habari, Meneja wa kampuni ya Mombasa Raha tawi la Mombasa Joseph Chengo aliilaumu NTSA kwa hasara hiyo.
“NTSA imetusababishia hasara kubwa sana ambayo hatuwezi kuirudisha kabisa,” alisema Chengo.
Aidha, alisema kuwa marufuku hiyo imesababisha kusimamishwa kazi kwa zaidi ya wafanyikazi 500 waliokuwa wakifanya kazi katika chama hicho cha ushirika hadi pale magari hayo yatakapoanza kuhudumu tena.
“Imebidi tuwasimamishe kazi wafanyakazi wetu hadi pale magari yetu yatarudi barabarani,” alisema Chengo.
Agizo la NTSA la kuondoa leseni ya chama hicho cha ushirika liliotelwa baada ya moja ya magari yake kuhusika katika ajali mbaya ya barabarani katika eneo la Kambu karibu na Makindu mwezi uliopita, ambapo watu zaidi ya 20 waliaga dunia huku 23 wakipata majeraha.
Siku ya Alhamisi Mahakama kuu ya Malindi ilitoa agizo la kukamatwa kwa Inspekta mkuu wa polisi nchini Joseph Boinnet, mwenyekiti wa NTSA Francis Meja, kamanda wa idara ya trafiki Jacinta Muthoni na afisa wa utekelezaji wa sheria wa NTSA Hared Adan kwa kwenda kinyume na agizo la mahakama la Mei 10 la kutoingilia utendakazi wa kampuni hiyo, hadi kesi iliyoko mahakamani itakapoamuliwa.