Serikali ya kaunti ya Mombasa imelitaka shirika la reli nchini kuharakisha zoezi la kuwafidia wavuvi walioathirika na ujenzi wa reli ya kisasa unaoendeelea.
Inasemekana kwamba ahadi ambayo wavuvi hao walipewa na shirika hilo takriban mika miwili iliyopita bado haijatimizwa na wavuvi hao wamekuwa wakiangaika kwani hawawezi tena kuendelea na uvuvi.
Akiongea na wanahabari ofisini mwake siku ya Jumatatu, waziri wa kilimo na uvuvi katyika kaunti hiyo Anthony Njaramba amesema kuwa wavuvi wengi wameathirika na shughuli ya uchimbaji mchanga baharini ambao unatumika katika ujenzi huo.
“Kampuni inayofanya ujenzi wa reli inachimba mchanga baharini kisha wanautumia katika ujenzi, lakini hatua hiyo imefanya wavuvi kushindwa kuendelea na kazi yao na sasa wanasubiri fidia hiyo ili wajikimu kimaisha,” alisema Njaramba.
Wakati huo huo waziri huyo aliongeza kuwa uchafu unaotokana na ujenzi huo hutupwa baharini na hali hiyo imechafua mazingira ya bahara na kusababisha samaki kutoroka maeneo ya kufanyia uvuvi.
“Tulianza mazungumzo na kampuni hiyo mwaka wa 2014 hadi kufikia sasa bado wavuvi hao hawajapata haki yao,” aliongeza.
Kampuni hiyo ya ujenzi wa reli ya kisasa ilianza kuchimba mchanga huo katika eneo la Waa kaunti jirani ya Kwale kabla kuhamisha shughuli zake na kuanza kuchimba sehemu ya Likoni Mombasa.
Kaunti ya Mombasa ina takriban wavuvi 1,700 waliosajiliwa na kulingana na waziri huyo ni kwamba hali hiyo ikizidi kuwa hivyo ni familia nyingi zinazoathirika kwani wanategemea biashara hiyo kujikimu kimaisha.
Majuma kadhaa yaliyopita wavuvi hao walielekea barabarani na kuandamana wakidai haki yao, na sasa serikali ya kaunti imeamua kuingilia kati kutatua tatizo hilo lililodumu kwa muda mrefu.