Share news tips with us here at Hivisasa

Kampuni ya usambazaji umeme nchini imepewa changamoto na wakazi wa kaunti ya Nakuru kuweka maafisa wa kukagua hali ya mashine na mitambo yao mara kwa mara ili kuzuia hasara na mikasa ya moto.

Meneja wa kampuni ya Royal Animal Feeds Limited Chege Mwaura amesema kwamba visa vya moto vinavyotokea katika kaunti ya Nakuru vimeongezeka, na vingine vinahusishwa na hitilafu za nguvu za umeme.

Chege alisema hayo baada ya moto mkubwa kutokea katika maghala ya viwanda vya shirika la wakulima la KFA, mjini Nakuru usiku wa Kuamkia Jumapili, na kusababisha hasara ya takriban shilingi milioni 100 kulingana na mkurugenzi mkuu wa KFA Bw Simon Cherogony.

Baadhi ya mali iliyoharibiwa na moto huo ni pamoja na magari na mashine za kutengeneza pamba.

Naye Judy Wacera, msimamizi wa kampuni ya unga ya Tit Food products, alisema hasara waliyopata ni kubwa mno kwani walikuwa wametoa bidhaa nchini Uganda siku moja kabla ya mkasa huo.

“Nilitoka Uganda kuleta bidhaa za kutengeza unga kama wimbi, lakini usiku saa nane nikapigiwa simu kwamba kuna moto katika viwanda vyetu, japo tulipofika tukapata kumeteketea na gare la kuzima moto lilikuwa likisaidia. Mlinzi wetu alisema kwamba kwanza stima ilipotea, na kisha moto ukazuka,” alisema Wacera.

Kulikuwa na baadhi ya wafanyikazi katika maghala hayo wakati moto huo ulipotokea japo hakuna aliyejeruhiwa.