Vita kati ya Idara ya Afya katika Kaunti ya Mombasa na kampuni za kuuza maji vimeonekana kuchukua mkondo mwingine baada ya kampuni hizo kutishia kufikisha idara hiyo mahakamani kwa kuwaharibia jina.
Mkurugenzi mkuu wa kampuni ya Starpop Abdi Omar amesema kuwa maji yao ni safi na yameidhinishwa na mamlaka ya kutoa idhini za bidhaa Kebs.
Aidha, mkurugenzi huyo alisema kuwa uchunguzi mwafaka haukufanyika kabla ya ilani hiyo kutolewa.
Kwa upande wake, mkurugenzi mkuu wa kampuni ya Wada Abdi Ahmed alisema kuwa idara hiyo haikufuata kanuni zote katika kufunga kampuni hizo, na kudai kuwa walipata ujumbe wa kufungwa kwa kampuni hizo kupitia kwa vyombo vya habari.
Hata hivyo, mkuu wa Idara ya Afya katika Kaunti ya Mombasa Abdi Mohammed amesema kuwa wametuma sampuli ya maji kutoka kwa kampuni hizo kwa waidhinishaji hao na watafanya uamuzi siku ya Jumanne.