Mwanamke mmoja ameishangaza mahakama moja ya Nakuru alipodai kwamba kang'ara aliyonaswa nayo na polisi ni dawa ya kutibu ng’ombe.
Akiwa mbele ya mahakama hiyo siku ya Ijumaa, Hellen Chepkemoi kutoka kaunti ndogo ya Njoro alidai kwamba lita tano za kang'ara alizonaswa nazo ni dawa ya kutibu ng’ombe wake anyeugua ugonjwa wa miguu na midomo almaarufu kama ‘foot and mouth’.
Akijitetea mbele ya hakimu mkuu Liz Gicheha kwa kukabiliwa na mashtaka ya kutengeneza na kuuza pombe hiyo ya kang'ara iliyoharamishwa, Chepkemoi alidai kwamba yeye hutumia kangara kama dawa ya kienyeji kwa kutibu mifugo wake wanapokuwa wagonjwa.
Licha ya kuomba mahakama hiyo imhurumie, Hakimu Gicheha alimuachilia kwa dhamana ya Sh20,000 au pesa taslimu Sh10,000 na mdhamini mmoja wa kiasi kama hicho.
Kesi hiyo itatajwa tena tarehe Oktoba 15 na kusikizwa tarehe Novemba 2, 2015.