Kanisa mbali mbali nchini zimehimizwa kudumu katika maombi ili Mungu kutuliza dhoruba kali ya mawimbi ambayo yanaendelea kuipiga nchi kila uchao na kutatiza uongozi na ustawi wa taifa.

Share news tips with us here at Hivisasa

Haya yalisemwa na Askofu Mkuu wa Jimbo la Kisumu wa Kanisa la Got Calvary Legion Maria Church, Askofu Isaac Benjamin Makokha wakati wa Ibaada ya kuadhimisha siku kuu ya Mtakatifu Paschal Baylon katika Kanisa la St. Mary's Immaculate mjini Kisumu mnamo siku ya Jumapili.

Akihutubu baada ya misa takatifu hiyo Jumapili, Askofu Makokha alitaja visa kadhaa vya mauaji ya kikatili ya raia waliouawa na kundi haramu la Al-Shabaab miezi michache ziliopita wakiwemo wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Garissa na walinda usalama, akisema kuwa uwepo wa Mungu umepungua baina ya wanadamu, hali ambayo inahitaji watu kumrejelea Mungu kwa kutubu na kusali.

“Tunapopungukiwa na utukufu wa Mungu ndipo maovu mengi yanapoinuka baina ya wanadamu na kusababisha maafa mengi. Hivo basi tunahitaji kudumu katika kusali na kuomba kama taifa ili Mwenyezi Mungu mwenyewe airehemu nchi,” alisema kiongozi huyo wa kanisa.

Askofu Makokha ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Kanisa hilo, alitoa wito kwa vyombo vya usalama nchini kuwajibika vikamilifu ili kuweza kuzuia maafa mengine zaidi ambayo yanatokea kwa sababu ya kuzembea kazini.

Aidha, Askofu huyo wa Jimbo la Kisumu aliitaka Serikali Kuu kuhakikishia raia wake usalama dhabiti kwa kuweka mikakati na mbinu mpya za kuimarisha usalama katika kila pembe za nchi, pamoja na kutunza hali ya mazingira ya vikosi vyake vya usalama.