Taarifa ya Naibu Msemaji wa IkuluIkulu ya Nairobi20 June, 2018
Hamjambo Mabibi na Mabwana,
Nafurahi kuwaona nyinyi nyote siku ya leo.
Mimi ni Kanze Dena, Naibu mpya wa Msemaji wa Ikulu.
Asubuhi ya leo tutaangazia masuala mbali mbali, yakizingatia shajara ya Rais Uhuru Kenyatta. Baada ya hayo nitasikiza masuali yoyote yatakayokuwepo.
Ziara ya Rais jijini Addis Ababa, Ethiopia,
Mnamo siku ya Alhamisi Kwanza kabisa, usalama wa kandaa hii ni muhimu sana kwa amani na maendeleo yetu ya kitaifa.
Kwa sababu hii, Rais – na taifa kwa jumla – anaendelea kuunga mkono juhudi za kuleta amani nchini Sudan Kusini.
Kesho (Alhamisi), Rais atajiunga na viongozi wengine wa kandaa hii huko jijini Addis Ababa, Ethioipia, kwa utaratibu wa mashauriano ya amani ya Sudan Kusini, ambao unaongozwa na shirika la IGAD.
Katika harakati za kuketa amani na uthabiti kwa jirani wetu wa Kaskazini, Kenya inashirikiana na itaendelea kufanya kazi kwa kuzingatia utaratibu wa shirika la IGAD. Tutaunga mkono maamuzi ya shirika la IGAD kuhusiana na hali ya Sudan Kusini.
Kenya imejitolea kuzingatia utaratibu wa kuleta amani na uthabiti Sudan Kusini na tutakuwa wapatanishi, wasioegemea upande wowote, chini ya utaratibu wa utendaji kazi wa IGAD.
Ziara ya Rais huko Ngong, Kaunti ya Kajiado, kukagua mradi wa Reli wa Standard Gauge Pili,
Mnamo siku ya Ijumaa wiki hii, Rais atazuru eneo la utendaji kazi la mradi wa reli ya Kisasa – yaani Standard Gauge (SGR) – katika Kaunti ya Kajiado.Katika muda wa miaka mitatu na zaidi, Rais amekuwa akifanya vikao mfululizo vya kila baada ya miezi mitatu kuhusiana na ustawi wa reli nchini.
Hii ni ishara ya kujitolea kwake kuimarisha muundo msingi, hatua ambayo ilichangia ufanisi wa uzinduzi na matumizi ya awamu ya kwanza ya mradi huu wa SGR.
Awamu ya 2A ya mradi huu itakuwa kupanua Reli hii kutoka Nairobi hadi Naivasha. Kwa ujumla tunaridhishwa na ufanisi uliofikiwa, ikiwemo kazi ya mpenyo wa umbali wa kilomita 4.5 kutoka Em-Bulbul katika Kaunti ya Kajiado.
Reli hii itachangia kwa kuafikia utaratibu bora wa haraka, adilifu na wa kutegemewa wa uchukuzi wa abiria na mizigo.
Mkutano Mkuu wa Ugatuzi
Tatu. Vile vile, mnamo siku hiyo hiyo ya Ijuma, Rais ataongoza Mkutano Mkuu wa Magavana. Rais amekuwa wazi kwamba yeye na magavana sharti wajadilie kinaga-naga jinsi Serikali ya Kitaifa na zile za Kaunti zinavyoweza kushirikiana kikazi kwa lengo la kuwanufaisha vilivyo na kuwaleta pamoja wananchi wa taifa hili.
Kwenye hotuba yake aliyotoa kwa Mkutano wa Magavana mwaka huu, Rais alisisitiza masuala matatu muhimu.
Kwanza, Kiongozi wa nchi alisema ni kulainisha uhusiano kati ya serikali ya kitaifa na zile za kaunti ili ziweze kutoa huduma zinazostahili badala ya kuzozana kuhusu mgao wa fedha.
Rais ataongoza majadiliano kuhusiana na masuala ya mikakati ya maendeleo yanayowahusu wananchi wetu.
Pili, Rais alisema – na bado ataendelea kusisitiza – kwamba wakati umewadia kufanya kazi, kuchuma mali na kuleta ufanisi kwa watu wetu. Siasa ziko na wakati wake.
Tatu, Rais akiwa anazingatia msingi wa kudumisha upatanishi, atajadili kwamba Wakenya wana shauku ya kusawazisha mikakati ya maendeleo ya kitaifa chini ya Ruwaza ya Maendeleo ya mwaka wa 2030.
Rais anatazamia kujadiliana kwa kina kuhusu masuala haya na Magavana. Ziara ya ujumbe mkubwa wa wafanyabiashara wa kutoka Marekani
Nne. Wiki ijayo ujumbe mkubwa wa wafanyabiashara wa Marekani utazuru Kenya kwa lengo la kuendelea kuimarisha uhusianao wa kibiashara, uekezaji na vile vile kuchunguza nafasi na njia mbadala zilizoko nchini.
Ujumbe huo utaongozwa na Katibu Mkuu (Under-Secretary) wa Biashara ya Kimataifa wa Serikali ya Marekani Gil Kaplan na wanachama wa Baraza la Rais wa Marekani la ushauri kuhusu Biashara barani Afrika.
Wakuu wa Makampuni na Mashirika makubwa-makubwa ikiwemo Bechtel, Visa, IBM, Overseas Private Investment Corporation, Acrow Bridge, Amethyst, Citi, GE, IBM, na mengine mengi pia watakuwepo katika ujumbe huo. Tunaukaribisha ujumbe huo hapa Kenya.
Tuko tayari kwa biashara na tunahimiza wafanyabiashara wa Marekani na wa mataifa mengine kuzuru na kuwekeza hapa Kenya na vile vile kushirikiana nasi kufanya kazi kwa mgao wa ufanisi ambao unajumuisha wote.
Asanteni.
Kanze Dena
Naibu Msemaji wa Ikulu