Tume ya uwiano na utengamano NCIC inapanga kuweka kamera za siri ili kuwanasa wanasiasa wanaotoa matamshi ya uchochezi na chuki.
Kulingana na mwenyekiti wa tume hiyo Francis Ole Kaparo, vifaa hivyo vitaigharimu serikali shilingi milioni 20.
Kaparo ameongeza kuwa visa vya matamshi ya uchochezi na chuki miongoni mwa wanasiasa vimezidi na huenda vikasabisha vita wakati wa uchaguzi ujao.
“Wanasaisa wengi wanajihusisha na visa vya matamshi ya uchochezi, hasa yaukabila,” alisema Kaparo.
Ameongeza kuwa vifaa hivi vitasaidia kukabiliana na visa vya ukabili, uchochezi na chuki nchini.
“Vifaa hivi vitaweza kunasa matamshi ya uchochezi yanayotolewa na wanasiasa nchini hasa wakati wa kampeni,” alisema Kaparo.
Pia wanapania kuweka vinasa sauti ambavyo vitasaidia kunasa sauti za uchochezi za wanasiasa hasa msimu huu wa uchugazi.
Wakati huo huo wanasiasa wanaowania viti mbalimbali wametakiwa kuondoa dhana kwamba kutakuwepo na udanganyifu wa kura katika uchaguzi huo akisema hilo ni kutayarisha wananchi kwa vurugu.
“Tuweni na uhakika wa kufaanyika kwa kura za usawa na haki, tukome kupiga domo kuwa uchaguzi ujao utakuwa wa wizi,” alisema Kaparo.
Ameyasema haya wakati wa kikao cha pamoja kilichohusisha kamati ya bunge kuhusu uwiano wa taifa pamoja na wadau wengine.