Share news tips with us here at Hivisasa

Ni mara nyingine tena ambapo msimu wa likizo umebisha hodi, na kama ilivyo ada, mji wa Mombasa hushuhudia watu kutoka kote nchini na hata katika mataifa ya nje wanaozuru Pwani ili kujivinjari.

Lakini sio wote wanaozuru eneo hili wakiwa na lengo moja tu la kujivinjari, wapo wengi ambao wana malengo fiche, la kwanza likiwa ni kuwaibia wenzao, kuwalaghai Wakaazi na hata kuna wale wanaowavizia watoto wadogo ufuoni na kuwatumia kingono.

Na ni kutokana na tathmini hiyo basi ambapo, nimechukua fursa hii kukukaribisha Mombasa mgeni mteule, kuna vyakula vingi tu, nisikugusie sambusa za nyama na viazi, kuna pilau, kuna biriani, kuna mishkaki ya maini samaki wa kupaka sijasahau ndio mandhari halisi ya Pwani haya.

Lakini ambacho hupaswi kukisahau usikimbilie ufuoni kama hujui kuogelea andamana na mtaalam unayemfahamu vyema, kama una familia yako kila mara andamana na familia yako, kama unaishi kwenye hoteli pata habari sahihi zinazohusiana na Mji wa Mombasa na ikilazimu andamana na Mfanyikazi wa hoteli ile.

Kuna visa ambavyo nimevishuhudia nikiwa mkaazi wa Mombasa, katika ufukwe wa Bahari Hindi wa Jomo Kenyatta al-maarufu Pirates huko Bamburi ambapo mabinti waliokuwa limbukeni wa maji ya bahari walifunzwa na wataalam ambao baadaye waliwabaka ndani ya maji hilo ulifahamu.

Hata hivyo, hupaswi kusahau mandhari ya joto ambalo katika juma lililopita limeruka kutoka vipimo vya nyuzi 28 hadi 33 hali inayowafanya wenyeji kushindwa kulala wakati wa usiku na kwako wewe japo itakuwa changamoto itakulazimu uzoe iwapo huwezani na mambo ya viyoyozi.

Tume hakikishiwa usalama wa kutosha na kamishna wa Kaunti ya Mombasa Nelson Marwa sambamba na kamanda mkuu wa polisi kaunti ya Mombasa na kote Pwani Francis Wanjohi ambao kwa kauli moja wamesema kwamba.

“Usalama hapa Pwani na hususan Kaunti ya Mombasa umeimarisha wenyeji na wageni hawana la kuhofia.”

Na mimi nakuambia karibu Mombasa, mandhari ya kuvutia, mandhari ya joto, lakini unachopaswa kuzingatia ni kwamba uwe mwangalifu kila wakati.

Karibu, na uwe na likizo njema.