Share news tips with us here at Hivisasa

Mwenyekiti wa chama cha Jubilee, tawi la Nakuru Bwana Karimi Waiganjo amewarai wakaazi wa kaunti ya Nakuru kuwa tayari kwa usajili wa wanachama ifikiapo Januari.

Akizungumza katika ofisi za TNA, Karimi amewataka wakaazi wa kaunti hii kukumbatia chama cha JPK ambacho ni imara zaidi kuliko kile cha awali kilichojulikana kama JAP (Jubilee Alliance Party).

Ametoa mwito kwa Rais Uhuru Kenyatta na naibu wake William Ruto, kuharakisha katika kumalizia kwa haraka kwa kuvunja vyama tanzu vya JAP.

Mkutano huo, uliohudhuria pia na viongozi mbalimbali toka mrengo wa TNA na URP, uliafikiana kuwa, watatoa orodha mpya wa jinsi ya kuwasajili upya wanachama wote wa chama cha JPK.

Kulingana na Karimi, viongozi wote walio serikalini watalazimika kujisajili tena kama wanachama wa JPK na wala hawatapewa kipaombele kwa dhana kuwa walikuwa ndani ya JAP hapo awali.

Karimi, amewasuta viongozi wa chama cha TNA tawi la Nakuru wakiongozwa na Harrison Muiruri kwa kutowajibika katika uongozi wa chama na kutoleta amani katika chama hicho kwani kilikuwa kimejawa na vurugu kila wakati. Hata hivyo Muiruri aliyekuwa amehudhuria hafla hiyo aliomba msamaha kwa wanachama na kusema atajisajili ndani ya JPK kama mwanachama mpya.