Waziri wa Wizara ya Jinsia na Vijana Cicily Kariuki amedhibitisha kuwa takriban shilingi milioni 180 za hazina ya vijana hazijulikani ziliko.
Akizungumza na wanahabari kwenye bustani ya Nyayo mjini Nakuru, Kariuki alisema kuwa wizara hiyo sasa imeagiza uchunguzi kamili ufanyike kubaini fedha hizo zilivyotumika.
Alisema kuwa mikakati kabambe imewekwa kuhakikisha fedha za kuwanufaisha vijana, wanawake na wale walio na ulemavu hazipotei.
Kariuki alisema sio vyema kuingiza siasa katika miradi muhimu ya serikali ambayo inalenga kuwanufaisha na kuwainua Wakenya kimaisha, na kuongeza kuwa lengo la serikali katika kubuni hazina hizo ni kuhakikisha kuwa hilo linatendeka.
“Nawahakikishia Wakenya kuwa fedha zenyu ziko salama na kuwa tumeweka mikakati ya kuhakikisha kuwa fedha hizo zinalindwa. Nawahakikishia kuwa sheria itachukua mkondo wake kuhusiana na fedha ambazo zimepotea za hazina ya vijana,” alisema Kariuki.
Kando na hayo, amewahakikishia wakaazi wa Nakuru kwamba miradi ya shirika la NYS iliyokuwa inawapa vijana wengi ajira itazinduliwa tena hivi karibuni.
Hata hivyo, amewataka Wakenya kuwa na subira huku wanapoweka mikakati mbalimbali ya kuhakikisha kuwa mradi huo unafanikiwa.
Kariuki ambaye pia alitoa hundi za thamani ya shilingi bilioni 32.2 kwa makundi 317 chini ya hazina za Uwezo, hazina ya vijana na ile ya Wanawake katika Kaunti ya Nakuru, kwa upande mwingine aliwahimiza vijana kutuma maombi ya kupata fedha hizo kwani idadi ya wale wanaoomba fedha hizo kwenye kaunti ya Nakuru iko chini.
Shughuli hii imejiri huku Kenya ikitarajiwa kuungana na dunia nzima katika kuadhimisha siku ya kimataifa ya Wanawake tarehe Machi 12, mwaka huu.
Matamshi yake yanajiri huku meneja wa fedha wa hazina ya vijana Benedict Etavachi kusema shilingi milioni 400 za hazina ya vijana hazijulikani ziliko.