Shirika la KARLO limeanzisha mpango wa kutoa chanjo dhidi ya magonjwa ya miguu na midomo, Lumpy Skin na homa ya Rift Valley katika eneo la Lanet.
Akizungumza na wakulima Jumatano, daktari Samwel Mbuku kutoka shirika hilo, alisema haya ni kufuatia mkurupuko wa ugonjwa unaosababishwa na virusi vinavyotokana na nyati vinavyodaiwa kuambukizwa kwa ng’ombe wanaozurura mjini humo kutafuta lishe na maji.
Dkt Mbuku alidokeza kuwa zoezi hilo linalenga zaidi ya wanyama mia nne na litaendelezwa kwa maeneo jirani ili kuthibiti afya ya wanyama na kuzuia maambukizi zaidi.
“Shirika letu liliweza kutoa chanjo sawia na hii kwa mifugo mapema Januari wakati kulizuka mkurupuko wa aina hiyo,” aliongeza Dkt Mbuku.
Wakati huo huo, daktari huyo alipuzilia madai kuwa takriban ng'ombe ishirini wameaga dunia kutokana na ugonjwa huo.