Aliyekuwa mbunge wa Gichugu Martha Karua, amesisitiza kuhusu umuhimu wa serikali kuhakikisha kuwa kuna usawa wa jinsia kwenye maswala ya uongozi na ajira nchini.
Akihutubia kongamano la pili la magavana linaloendelea kwenye chuo cha Leba cha Tom Mboya jijini Kisumu, Karua amesema licha ya katiba kuwajali na kuwatambua wanawake, usawa wa jinsia bado haujatekelezwa kikamilifu katika sekta zote za serikali kuu na zile za kaunti.
“Nataka kutoa changamoto kwa serikali ya muungano wa Jubilee, ambayo ina manifesto bora zaidi kuwahusu wanawake.
Kilichosalia sasa ni serikali kuhakikisha kuwa manifesto hiyo imetekelezwa kikamilifu, ili kufanikisha usawa wa jinsia nchini,” akasema Karua.
Karua ambaye aliwania urais kwenye uchaguzi mkuu uliopita na kupoteza, amesema kuwa wanawake wana jukumu la kuwania nafasi za uongozi, akisema hiyo ndio njia pekee ya kushindana na wanaume kisiasa.
Matamshi yake yaliungwa mkono na seneta wa jimbo la Kakamega daktari Bonny Khalwale, ambaye ni miongoni mwa maelfu wa viongozi na wajumbe wanaohudhuria kongamano la pili la magavana kuhusu ugatuzi jijini Kisumu.
Kati ya magavana 47 hakuna mwanamke.
Aidha, miongoni mwa maseneta 47 hakuna mwanamke hata mmoja, isipokuwa maseneta wateule; walioteuliwa na vyama vya siasa baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2013