Wanawake katika Kaunti ya Mombasa wamehimizwa kujitokeza na kugombea viti vya uongozi kwenye uchaguzi mkuu ujao.

Share news tips with us here at Hivisasa

Akiongea mjini Mombasa siku ya Jumatatu, kwenye kongamano la kujadili maswala yanayokumba uongozi wa wanawake, Kinara wa chama cha Narc Kenya Martha Karua alisema kuwa iwapo wanawake watajitokeza kikamilifu, lazima swala la uongozi litatekelezwa.

Karua amewahimiza wanawake kujitokeza na kuwania viti mbalimbali vya uongozi.

Kiongozi huyo alisema kuwa hatua hiyo itaboresha uongozi wa nchi pamoja na kubadilisha uongozi wa kiimla unaoshuhudiwa kwa sasa.

Bi Karua alisema kwamba jamii inafaa kuondoa kasumba ya tamaduni zilizopitwa na wakati na kuutambua uongozi wa wanawake.

"Kuna umuhimu wa wanawake kujitokeza na kuwania nyadhifa mbalimbali za uongozi na kuleta mabadiliko nchini,” alisema Karua.

Wakati huo huo, kiongozi huyo amelikosoa bunge la kitaifa kwa kushindwa kuupitisha mswaada wa usawa wa jinsia na kutaja hatua hiyo kama ukiukaji wa katiba.