Share news tips with us here at Hivisasa

Wakazi wa Kiamabundu wadi ya Kisii, eneo bunge la Nyaribari Chache Kaunti ya Kisii wamempongeza Kasisi Lawrence Nyaanga kwa juhudi zake za kumwaga pombe haramu katika eneo hilo.

Wakiongea siku ya Jumatatu katika kijiji cha Etangi-Kiamabundu, baadhi ya wakazi hao walimpongeza kasisi huyo kwa kazi anayoendelea kufanya ya kumwaga pombe haramu na kusema kuwa pombe hiyo imekuwa ikiwasumbu kwa muda mrefu.

Haya yanajiri baada ya kasisi huyo kufika katika eneo hilo siku ya Jumapili na kumwaga pombe katika eneo hilo.

Aidha, wamewaomba viongozi wengine haswa maafisa wa polisi kushirikiana na kasisi huyo ili kuhakikisha kuwa agizo la Raisi la kumaliza pombe haramu limezingatiwa katika kijiji hicho.

Wakazi hao walisema kuwa pombe hiyo imewafanya vijana wengi kuacha shule na kujihusisha na visa vya wizi katika eneo hilo.

“Nampongeza kasisi kwa kuchukua hatua hiyo ambayo wengi wanaona kuwa haina umuhimu. Hiyo ni njia mojawapo ya kusaidia vijana na wazee wetu kwa kuwa wengi wamejihusisha na unywaji huo,” alisema, Florence Bosire mkaazi.

Kwingineko, naibu chifu wa eneo hilo George Nyamwaka aliombwa kuungana na kasisi huyo ili kuhakikisha kuwa pombe hiyo imeisha.

“Namuomba Naibu chifu wetu kuungana na Kasisi Lawrence ili pombe hii iweze kuisha katika eneo hili kwani hata familia nyingi zimevujika kwa sababa ya pombe hiyo," alisema Edwin Nyabuto, mkazi.