Siku mbili tu baada ya serikali ya kitaifa kudinda kuwapa wafanyakazi nyongeza ya mishahara kwenye hafla ya kuadhimisha siku ya wafanyakazi ulimwenguni, sasa katibu mratibu wa chama cha mashamba makubwa makubwa nchini Henry Omasire ameshtumu vikali hatua hiyo. 

Share news tips with us here at Hivisasa

Akiwahutubia wanahabari mjini Nyamira siku ya Jumanne, Omasire alisema amesikitishwa na hatua hiyo ya serikali kutowapa wafanyakazi nyongeza ya mishahara ikizingatiwa wafanyakazi huchangia pakubwa katika uimarishaji wa uchumi nchini.

"Ni jambo la kushangaza kwamba tunaweza adhimisha siku ya wafanyakazi ulimwenguni na kisha serikali kuu ikatae kabisa kutangaza nyongeza ya mishahara kwa wafanyakazi ilhali wafanyakazi huchangia pakubwa katika uimarishaji wa uchumi nchini," alishangazwa Omasire. 

Omasire aidha alisema kwamba vyama vya wafanyakazi nchini vitafanya kongamano la pamoja kule Kisumu tarehe 21 mwezi huu waMei ili kuzungumzia suala hilo huku pia akiishtumu serikali ya Jubilee kwa ufisadi.

"Sisi viongozi wa mashirika mbalimbali ya wafanyakazi tutajumuika jijini Kisumu tarehe 21 mwezi huu chini ya mwavuli wa COTU ili kujadili suala hili kwa undani, kwa maana tumegundua kwamba inachozingatia serikali ya Jubilee ni wizi wa mali ya umma na wala sio kubuni nafasi za kazi," aliongezea Omasire.