Katibu wa wizara ya afya katika serikali ya kaunti ya Nyamira Douglas Bosire amewaonya vikali wahudumu wa afya wanaojihuzisha na wizi wa madawa.
Kwenye mahojiano ya kipekee siku ya Jumanne, Bosire alisema kuwa ni aibu kwamba baadhi ya wahudumu wa afya katika zanahanati na hospitali za kaunti hiyo hujihuzisha na wizi wa dawa za hospitalini.
"Ni jambo la aibu sana kwamba baadhi ya wahudumu wa afya hujihuzisha na wizi wa dawa kutoka kwa zahanati na hata hospitali za kaunti, dawa ambazo zafaa kuwatibu wagonjwa," alisema Bosire.
Bosire aidha aliongeza kuwa wizara ya afya imeweka mikakati ya kufanya upekuzi kwenye hifadhi za dawa kwenye vituo vya afya vya serikali ili kubaini iwapo kuna dawa zitakazopatikana kuibiwa, huku pia akionya wahusika kuachishwa kazi zao.
"Kama wizara tumeweka mikakati ya kufanya upekuzi wa hifadhi za madawa kwenye zahanati na hospitali za kaunti ili kubaini iwapo kuna dawa za aina yeyote zilizoibiwa, na ukweli ni kwamba yeyote atakayepatikana kuhusika ataachishwa kazi mara moja," aliongezea Bosire.