Katibu mkuu wa chama cha shirikisho la madiwani nchini KNCF Tom Mboya amejitokeza kuitaka serikali ya kitaifa kuwalipa madiwani wa zamani kote nchini shillingi millioni 1.5 kama kiinua mgongo kwa kulihudumia taifa hili.
Akiwahutubia wanahabari kwenye mkahawa mmoja mjini Nyamira siku ya Jumapili baada ya kufanya mkutano wa pamoja na madiwani zaidi ya mia mbili kutoka eneo hilo, Mboya alisema serikali yastahili kulipa madiwani shillingi elfu 30 kila mwezi, huku ikiwapa marupupu ya kimatibabu.
"Sisi shirikisho la madiwani wa zamani nchini tunaitaka serikali ya kitaifa iwalipe madiwani waliostaafu shillingi millioni 1.5 kama zawadi kwa kujitolea kwao kulihudumia taifa hili na pia ihakikishe kwamba wanapata mshahara wa elfu 30,000 kila mwezi," alisema Mboya.
Mboya aidha alizitaka serikali za kaunti kuwaruhusu madiwani wa zamani kuhudhuria vikao vya mabunge ya kaunti bila yao kusumbuliwa.
"Baadhi ya madiwani wa zamani wamekuwa wakiwasilisha lalama kwamba serikali zingine za kaunti haziwapi nafasi ya kuhudhuria vikao vya bunge, ila ni ombi letu kwa serikali husika kuwaruhusu madiwani kuhudhuria vikao hivyo na hata ikiwezekana wateuliwe kuhudumu kwenye kamati mbalimbali," aliongezea Mboya.