Katibu mratibu wa chama cha mashamba makubwa makubwa nchini Henry Omasire amejitokeza kushtumu vikali maombi ya kitaifa yaliyoandaliwa na Rais Kenyatta kwenye uwanja wa Afraha siku ya jumamosi. 

Share news tips with us here at Hivisasa

Kwenye mahojiano na kwa njia ya simu, Omasire aliusuta mkutano huo wa maombi huku akiutaja kama kejeli kwa waathiriwa wa ghasia za baada ya uchaguzi wa mwaka wa 2007 ambao bado wangali kufidiwa. 

"Ni aibu kubwa kwamba Rais Uhuru Kenyatta anaweza andaa mkutano wa maombi kule Nakuru ili kushukuru kwa sababu ya kukamilika kesi za jinai zilizokuwa zikimkabili naibu wake na mtangazaji Joshua Sang ilhali maelfu ya waathiriwa wa ghasia za baada ya uchaguzi hawajafidiwa hadi sasa," alisema Omasire.

Omasire aidha alimtaka Rais Kenyatta kuweka mikakati ya kuhakikisha kuwa waathiriwa wa ghasia za uchaguzi wa mwaka 2007 wamefidiwa ili kurejelea maisha yao ya kawaida. 

"Ni jambo la kushangaza kwamba miaka tisa baada ya ghasia za uchaguzi kuna wakenya ambao bado wangali wanaishi kwenye hema huku mikutano ya maombi iliyoigharimu serikali mamillioni ya pesa ikiandaliwa na ndio sababu sharti rais Kenyatta ahakikishe kuwa waathiriwa wa ghasia wamefidiwa kwa haraka," aliongezea Omasire.