Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Katibu mkuu wa chama cha KNUT tawi la Nyamira Nicholas Nyang’au amekashifu matamshi ya mwenyekiti wa tume ya kuajiri walimu nchini TSC Lydia Nzomo kuwa walimu warudi darasani la sivyo wasimamishwe kazi.

Katibu huyo alisema Nzomo hajui ni hatua zipi zinastahili kufuatwa ili kusimamisha walimu kazi nchini ila ni kuongea anaongea huku akisema kilio cha chura hakiwezi kumzuia ng’ombe kunywa maji.

Nyang’au alisema mgomo wa walimu unaoenedelea kushuhudiwa nchini kwa sasa ni halali na utazidi kuendelea hadi walimu waongezwe mshahara wao jinsi mahakama ilivyoagiza.

Akizungumza na wanahabari siku ya Jumapili mjini Nyamira, Nyang’au alisema hakuna mwalimu ataenda darasani katika kaunti ya Nyamira na mgomo utaendelea hadi pale watakapolipwa nyongeza ya mishahara.

Katibu huyo alisema vitisho vya Lydia Nzomo haviwezi kusitisha mgomo wa walimu nchini.

“Kufikia sasa sisi walimu tumemla ng’ombe mzima. Kwani mkia utatushinda kweli?” auliza katibu Nyangau.

Matamshi ya katibu huyo yaliungwa mkono na katibu Peter Munde wa Borabu ambaye alipongeza walimu kwa kuitikia ombi la chama cha KNUT kuendelea kugoma hadi walipwe mshahara.

“Tutaendlea kugoma. Yale ya Lydia Nzomo hayawezi kututisha kamwe mpaka serikali ituwekee mishahara yetu kwa akaunti zetu,” alisema Munde.