Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Serikali kupitia Wizara ya Afya imesema tayari imefaulu kupeana vifaa vya matibabu katika kaunti 24 humu nchini, huku zoezi hilo likiendelea katika kaunti zilizosalia.

Waziri wa Afya Cleopas Mailu amesema kuwa zoezi hilo linaendelea katika kaunti zote na wizara yake itahakikisha kuwa hospitali zote katika kila kaunti zinapokea vifaa hivyo.

Akiongea katika kikao na wanahabari katika hoteli ya Mombasa Beach mjini Mombasa siku ya Jumatatu, Mailu alisema mpango huo ulioanza mwezi Mei mwaka jana uliratibiwa kukamilika katika kipindi cha mwaka mmoja.

“Serikali iliweka mpango wa kutoa vifaa mbalimbali vya kusaidia huduma za matibabu katika hospitali za kaunti. Tunatarajia ifikiapo mwezi Juni mwaka huu, tutakuwa tumekamilisha zoezi hilo,” alisema Mailu.

Waziri Mailu alisema kuna takriban hospitali 96 katika kaunti zote nchini ikijumuishwa na zile za rufaa.

Hata hivyo, waziri huyo alisema kumekua na changamoto kubwa katika baadhi ya kaunti hasa katika upande wa miundo mbinu ya hospitali.

“Kaunti mbalimbali zilikuwa na miundo mbinu duni wakati tulipoanza mpango huu, kwa hivyo baadhi ya hospitali zitasubiri lakini tunatumai ifikiapo mwisho wa mwaka huu, mambo yatakuwa sawa,” aliongeza Mailu.

Kati ya hospitali zinazotarajiwa kufaidika na mpango huo wa kutoa vifaa vya matibabu ni hospitali kuu kanda ya Pwani ya Coast General inayotegemewa na wakaazi wengi.