Gavana wa jimbo la Nakuru Kinuthia Mbugua amekiri kuwa serikali yake inakabiliwa na changamoto za uhaba wa vifaa vya kukabiliana na mikasa ya moto inayotokea katika jimbo hilo.
Hayo ni kufuatia shutuma kali kutoka kwa wakaazi dhidi ya serikali ya kaunti ya Nakuru, baada duka moja la kuuza vifaa vya ujenzi kushika moto wikendi eneo la Viwandani, ambapo gari la kuzima moto la jimbo lilichelewa kufika mahala pa tukio huku mali ya mamilioni ya pesa ikiteketea.
Gavana alisema hatapuzilia mbali ripoti zilizoandikwa na vyombo vya habari kuhusu kuchelewa kwa zima moto, huku akimwelekeza waziri wa miundo msingi Joel Maina Kairu kuhakikisha kwamba vifaa vyote vya kukabiliana na moto katika kaunti vinafanya kazi.
Hata hivyo amesema kuwa serikali yake kwa sasa ina magari mawili pekee ya kutoa huduma hiyo katika kaunti ndogo zote 11.
Mbunge wa Nakuru mashariki Samwel Arama alikuwa mmoja kati ya waliokemea kuchelewa kwa gari hilo la kuzima moto.
“Japo tuna matatizo na upungufu huu, isionekane kana kwamba serikali ya kaunti yetu imeshindwa kukabiliana na majanga ya moto yanayaotokea” Mbugua alisema.