Waziri wa utawala katika kaunti ya Kisii Peris Onsarigo amesema serikali ya kaunti hiyo itaandaa vikao katika kila eneo bunge la kaunti hiyo hivi karibuni kukusanya mahitaji ya wakazi wa kaunti kuhusu wanayoyahitaji kutendewa.

Share news tips with us here at Hivisasa

Kulingana na waziri huyo, ni vyema kupata mahitaji ya wananchi ili kufuata utaratibu wa kufanya maendeleo kila sehemu ya kaunti, huku akisema vikao hivyo vitatumika na serikali kueleza maendeleo ambayo imetekeleza tangu serikali za ugatuzi kuanzishwa nchini.

Akizungumza siku ya Jumanne mjini Kisii, Onsarigo aliomba wakazi wa kaunti hiyo kushirikiana na viongozi wa kaunti kuleta maendeleo zaidi, huku akisema wataandaa vikao kujua yale wakazi wanahitaji kufanyiwa.

“Ni vizuri sisi sote kati ya viongozi na wakazi kushirikiana kusongesha kaunti yetu mbele kimaendeleo, kaunti itaandaa vikao hivi karibuni katika maeneo bunge yote tisa kukusanya mahitaji ya maendeleo ili kaunti yetu kusonga mbele kimaendeleo,” alisema Onsarigo.

Onsarigo aidha aliiongeza kuwa ni haki kwa mwananchi kujua jinsi serikali inatumia pesa za bajeti, na kusema mwananchi anastahili kuhusishwa katika maendeleo.

Mahitaji ambayo yatatolewa yataunganishwa na mahitaji ya wakazi wa kaunti zingine 46 katika mkutano wa ugatuzi ambao utaandaliwa katika kaunti ya Meru mwezi huu.