Wafugaji katika Kaunti ya Mombasa wanatarajiwa kufaidika na mradi wa chanjo kwa mifugo unaonuiwa kuanzishwa na serikali ya kaunti.
Mradi huo ambao utaandaliwa mwezi ujao utawajumuisha madaktari kutoka Wizara ya Kilimo ambao wataungana na wale wa kaunti kutoa matibabu hayo sawia na mafunzo ya kuwalinda mifugo ikiwemo yale ya kutambua magonjwa.
Akizungumza na waandishi wa habari kwenye afisi yake, mkuu wa idara ya kilimo na mifugo Kaunti ya Mombasa Anthony Njaramba, alisema idara yake imeafikiana kuanzisha matibabu ya mifugo kutokana na shinikizo zilizotolewa hivi karibuni na baadhi ya wafugaji katika eneo la Mwakirunge, eneo linaloaminika kuchangia pakubwa kwa bidhaa ya maziwa yanayouzwa kwenye mabohari ya maziwa Mombasa.
Njaramba aliyekuwa ameandamana na wanachama kutoka miungano mbalimbali ya wakulima, alisema kuwa idara hiyo iko kwenye mchakato wa kutafuta namna ya kutoa dawa za mifugo kwa wakulima, hususan msimu huu ambapo mvua inatarajiwa kuanza kunyesha.
Kwa upande wa mafunzo, Njaramba alisema kuwa baada ya matibabu hayo, idara ya kilimo pia itaandaa warsha itakayowaleta pamoja wakulima wa aina mbalimbali ikiwemo wale wanaopanda mboga na matunda, ili kuwajuza kuhusiana na athari za mvua kwa afya ya mifugo na mimea.
Njaramba amewasihi wakulima kushirikiana na serikali ili kuhakikisha kuwa zoezi hilo linatekelezwa kikamilifu punde tu litakapong’oa nanga mwezi ujao.