Mkurugenzi mkuu wa Shirika la Haki Afrika amesema kuwa wamezindua mradi wa kukusanya maoni ili kuunda sera maalum ya jinsi ya kukabiliana na ugaidi katika Kaunti ya Mombasa.
Hussein Khalid amesema kuwa vita dhidi ya ugaidi vimetekelezwa kinyume na maadili ya haki za kibinadamu na sheria.
Akizungumza mjini Mombasa siku ya Jumamosi, Khalid alisema kuwa shirika hilo limewapatia wakaazi nafasi ya kutoa maoni yao ili kubuniwa kwa sera hiyo itakayosaidia kudhibitiwa kwa maswala ya ugaidi na itakadi kali.
Khalid alisema kuwa iwapo wakaazi wa Kaunti ya Mombasa watashirikiana na shirika hilo na kutoa maoni yao, basi sera hiyo itasaidia katika kuhakikisha kuwa vita dhidi ya ugaidi vinatekelezwa kwa kuzingatia haki za kibinadamu.
“Tunaimani kuwa iwapo wakaazi watashirikiana na shirika letu basi kwa kiwango kikubwa maoni tutakayokusanya yatasaidia kudhibiti ugaidi na uhalifu kwa kiwango kikubwa,” alisema Khalid.
Khalid alifichua kuwa wakaazi waliojitokeza kutoa maoni yao kuhusiana na swala la ugaidi, wameishinikiza serikali kuu kushirikiana nao moja kwa moja ili kufanikisha vita hivyo.
Mchakato huo wa kubuni sera ya kupambana na ugaidi katika Kaunti ya Mombasa unatarajiwa kukamilika katika kipindi cha majuma matatu yajayo, ili sera hiyo ianze kutumika rasmi.