Serikali ya kaunti ya Kisii imetangaza kuchima visima vya maji kwa kila wadi ya kaunti hiyo.
Hii ni baada ya idadi nyingi ya wakaazi kupendekeza kuwekewa mradi wa maji kwani wengi husumbuka kutafuta maji hayo kwa kutembea mbali kuyatafuta.
Akizungumza siku ya Jumanne katika eneo la Amasago wakati wa kusherekea siku ya maji, afisa wa mazingira na maji katika kaunti ya Kisii Zablon Ongori alisema serikali ya kaunti imeweka mikakati kabambe ya kuchimba visima kwa kila wadi kabla ya mwaka huu kukamilika.
“Serikali ya Kisii itachimba visima kutoa usaidizi kwa wakaazi kabla ya mwaka huu kukamilika ili wakaazi wafaidike na mradi huo wa maji ambao umekuwa changamoto kwa wakaazi wengi,” alisema Ongori.
“Kufikia sasa serikali imechimba visima 25 na tutachima visima 29 kwa kila wadi na kuyaunganisha kwa shule, masoko na wakaazi,” aliongeza Ongori.