Gavana wa Kaunti ya Taita Taveta Granton Samboja akiwahutubia wanahabari hapo awali. [Picha/ the-star.co.ke]
Wafanyabiashara katika Kaunti ya Taita Taveta huenda wakanufaika pakubwa kutokana na hatua ya serikali ya kaunti kuanzisha ushirikiano wa kipekee na shirika la akiba na mikopo la Qwetu Sacco.Kupitia kwa Gavana Granton Samboja, serikali ya kaunti ya Taita Taveta imeanzisha mradi wa kuwadhamini wafanyabiashara wadogo wanaohitaji mikopo ili kujiendeleza.Gavana Samboja amesema kuwa hatua hiyo itapelekea watu wengi kujitosa katika biashara, jambo ambalo amesema litaboresha pakubwa uchumi wa kaunti."Nataka watu wangu wa kaunti hii watoke katika maisha ya kungoja kupewa pesa na wanasiasa, waingie katika maisha ya kujitafutia riziki yao," alisema Samboja.Samboja alisema kuwa kaunti hiyo itaimarika iwapo kutakuwepo na watu wengi wanaofanya biashara na kilimo.Gavana huyo alisema kuwa maafikiano kati ya serikali yake na shirika la Qwetu Sacco yatawasaidia pakubwa kina mama, vijana na watu wanaoishi na ulemavu kwani makundi hayo yamekuwa yakilalamikia kukosefu wa fedha kama changamoto kuu ya kutofanya biashara.Kwa upande wake, mkurugenzi wa wa shirika hilo Charles Kaba amesema wanamalengo ya kupanua huduma zao kufika kaunti zote inchini.Kaba alisema japo shirika hilo lilianzishwa na walimu wa Kaunti ya Taita Taveta, wamefungua milango kwa umma na hasa watu wanaotaka kufanya biashara au ukulima."Tumefanya uchunguzi na utafiti mjini Mombasa na hivi karibuni tutaanzisha tawi lingine huko. Tunalenga kupata wateja wengi zaidi ili tuweze kuimarisha zaidi huduma zetu," alisema Kaba.Aidha, Kaba amesema vijana wengi wamekuwa wakikwepa kuchukua mikopo kutokana na ukosefu wa wadhamini, na kutoa wito kwa vijana kujitokeza kwa wingi kwani sasa serikali itawahakikishia usalama wa mali yao wanapochukua mikopo hiyo.