Katibu wa Kaunti ya Mombasa Bwana Francis Thoya amesema kuwa kaunti hiyo imeweka mikakati ya kujenga kiwanda cha kusaga taka.
Akiwahutubia wanahabari mjini Mombasa siku ya Alhamisi, Thoya alisema kuwa suala la taka limekuwa kero kwa wakaazi, huku akiongeza kuwa ipo haja ya changamoto hiyo kutatuliwa kwa haraka.
“Kaunti inakusudia kujenga kiwanda cha kusaga taka na kufanya utumizi mpya wa taka hizo. Mji umekua haraka huku watu wakiongezeka, hatua iliyofanya taka kuongezeka kwa hali ya haraka sana,” alisema Thoya.
Katibu huyo alisema kuwa tayari serikali ya kaunti imefanya mazungumzo na baadhi ya wawekezaji walio na nia ya kujenga kiwanda hicho.
“Wawekezaji tayari wamefanya kikao na idara husika na hivi karibuni tutatangaza zabuni hiyo ili kutuwezesha kupata kampuni itakayosimamia mradi huo,” aliongeza.
Aidha, Bwana Thoya amesema kuwa Halmashauri ya viwanja vya ndege KAA, imeonya kaunti dhidi ya utumizi wa jaa la Mwakirunge, kwa madai kuwa inazuia njia ya ndege.
“KAA imetuandikia barua ikituomba kufunga jaa la Mwakirunge. Halmashauri hiyo imezua wasiwasi kuwa ndege wanaokuwa katika jaa hilo huenda wakaingia katika injini ya eropleni na kusababisha ajali,” alisema Thoya.