Gavana wa Kaunti ya Kisii James Ongwae amesema kila mwaka serikali yake itakuwa inajenga madarasa mawili ya chekechea katika wadi zote zilizoko katika kaunti hiyo.
Hii ni baada ya serikali za ugatuzi kukubaliwa mamlaka ya kusimamia sekta hiyo ya masomo ya watoto wa chekechea katika shule mbalimbali.
Akizungumza siku ya Alhamisi katika mji wa Kisii, Gavana Ongwae alikiri kuwa atahakikisha viwango vya elimu vimeimarika zaidi katika shule mbalimbali za kaunti hiyo haswa katika masomo ya watoto wa chekechea.
Ongwae alisema kuwa shule za chekechea ndizo msingi wa elimu kwa kila mtu asomaye humu nchini.
“Kila mwaka nitajenga madarasa mawili ya chekechea katika kila wadi. Kaunti yangu iko na wadi 45 kumanisha nitajenga madarasa 90 kwa kaunti nzima kwa kila mwaka mpaka nitakapotoka mamlakani kama njia mojawapo ya kuinua viwango vya elimu,” alisema Ongwae.
Aliongeza: “Nahitaji msingi uwe mwema kwa watoto wetu ili nao waje kufurahia masomo kupitia matunda ya serikali za ugatuzi.”
Wakati huo huo, Gavana Ongwae alisema serikali ya kaunti yake imeajiri walimu ambao watakuwa wakiwafundisha watoto wa chekechea.
Aliwaomba walimu hao kuwasomesha watoto hao kwa motisha ili wawe wanapita na kukielewa kile wanachofundisha.
“Naomba kila mwalimu afundishaye katika darasa za chekechea ajitiolee tusaidie watoto wetu wachanga maana hapo ndipo msingi wa watoto upo. Watoto hao ndio watakuwa viongonzi wa kesho maana sisi tutaondoka. Tusipowasomesha nani atakuwa kiongozi?Nawaomba tuwafundishe watoto kwa bidii,” alisema Ongwae.