Huku wakaazi wengi wakiwa hawana uwezo wa kugharamia matibabu ya hospitali, kaunti ya Kisii imeahidi kununua bima kwa wakaazi elfu 40.

Share news tips with us here at Hivisasa

Ahadi hiyo imetolewa na Gavana James Ongwae alipokuwa akihutubia wananchi katika ukumbi wa Cultural Hall mjini Kisii kuhusiana na mipango na hatua serikali yake imepiga tangu kuingia mamlakani.

Bwa Ongwae alisema kuwa atashirikiana na wasimamizi wa kila wadi ili kupyiaa kati ya watu 800 hadi 1000 kutoka kwa kila wadi huku akisema kuwa wameshakubaliana na wawakilishi wa wadi kuweka mswada bungeni na kuupitisha ili kujumuishwa katika bajeti ya mwaka huu na ule ujao(2015/2016).

"Kila wadi itawasilisha kati ya watu 800 hadi 1000 na tutahakikisha ni wale watu hawajiwezi kabisa. Tunataka kufanikisha yote haya kupitia kwa wasimamizi wa wadi ili kuepuka watu kuweka jamaa zao wanaojiweza," Ongwae alisema.

Gavana alisema kwamba hii itasaidia wananchi kupata huduma hospitalini, kwa wale ambao hawajakuwa na uwezo huo.

Pia Ongwae alionyesha furaha yake kwa kuwashukuru mawaziri, maafisa wakuu katika wizara na kuwapongeza wawakilishi wa wadi zote katika kaunti hiyo kwa kuwa karibu naye kufanya kazi ya maendeleo.