Serikali ya Kaunti ya Mombasa imesema kuwa iko katika mikakati ya kununua ekari 3,000 za ardhi katika sehemu za kaskazini, kusini na magharibi mwa Pwani ili kuvutia wawekezaji katika kufanya biashara na serikali ya kaunti hiyo.

Share news tips with us here at Hivisasa

Akizungumza siku ya Jumatatu, Katibu wa Kaunti ya Mombasa Francis Thoya alisema kuwa ardhi hizo zitanunuliwa katika sehemu ya Dogo Kundu huko Miritini, na eneo la Mwakirunge.

Thoya alisema kuwa ardhi hizo zitanunuliwa kama matayarisho ya miradi itakayogharimu milioni kadhaa ya pesa, ambayo inatarajiwa kuanzishwa hivi punde katika kaunti hiyo.

“Hatutaki wakati ambapo wawekezaji wanapofika ndipo tunaanza kukimbia juu chini tukitafuta ardhi ya kuanzisha miradi tofauti,” alisema Thoya.

Katibu huyo alisema kuwa serikali ya Kaunti itahitaji takriban bilioni moja katika kununua ardhi hizo, huku akiongeza kuwa fedha hizo zitapitishwa katika bajeti ya mwaka wa 2016/2017.