Kutokana na mswada wa elimu wa mwaka elfu mbili na kumi na tatu unaohakikisha kwamba shule zote nchini zinasajiliwa upya, mkurugenzi wa maswala ya elimu kaunti ya Uasin Gishu Rebecca Butalanyi amesema kuwa wamepewa hadi tarehe kumi na nne mwezi wa Julai mwaka huu, kuhakikisha kwamba shule zote za umma na zile za kibinafsi zinasajiliwa.

Share news tips with us here at Hivisasa

Akizungumza siku ya Jumatatu katika ofisi yake, Butalanyi alisema kwamba wao kama kaunti wamejizatiti kuhakikisha kuwa shule zote katika kaunti hiyo, ziwe za msingi au sekondari za umma au kibinafsi zimesajiliwa ifikapo siku hiyo.

Aidha, alihoji kuwa kabla ya shule kusajiliwa, ni muhimu kutimiza malengo yaliyo kwenye mswada huo, ikiwemo shule kuwa na barua kutoka wizara ya afya ya umma, ripoti ya Nema, kipande cha ardhi kiwe cha kutosha kwa wanafunzi, haswa wa kucheza na pia darasa iwe ya kutosha zaidi ya wanafunzi arobaini.

Vile vile, shule hiyo iwe imezungukwa na ua na iweze kuwajali wanafunzi wenye ulemavu.

Kando na hayo, alisema kwamba hakuna shule yoyote ya kibinafsi itakayosajiliwa ikiwa mwenye shule hiyo atakua ameshtakiwa kwa kosa dhidi ya watoto, mwalimu aliye katika shule hiyo hajajisajilisha na tume ya kuajiri walimu (TSC), na ikiwa mmiliki hastahili kuwa kati ya wamiliki kulingana na kifungu cha sita cha katiba.

Aliongeza kuwa shule hizo zitakaguliwa mara kwa mara hata baada ya kupewa vyeti ili kuhakikisha viwango vya elimu ni ya juu.