Serikali ya kaunti ya Nyamira itatoa mafunzo kwa wakazi wa kaunti hiyo jinsi ya kufanya upanzi wao kuepuka hasara inayosababishwa na mvua nyingi.

Share news tips with us here at Hivisasa

Hii ni baada ya kubainika kuwa wengi wa wakulima wanapofanya upanzi wao hawazingatii na kufuata njia zinazostahili ili mvua inaponyesha isije ikaharibu wanachopanda katika mashamba yao.

Akizungumza siku ya Jumatatu mjini Nyamira, afisa wa kilimo katika kaunti ya Nyamira Edward Ondigi alisema serikali imejiandaa ili kutoa mafunzo kwa wakazi ili kujua jinsi watafanya upanzi wao kuepuka hasara inayosababishwa na mvua.

“Mvua ambayo hunyesha huaribu mimea ya wengi na kusababisha hasara, lakini serikali yetu itatoa mafunzo kwa wakazi kujua ni kipi watapanda na kwa njia gani watafanya upanzi huo,” alisema Ondigi.

Wakati huo huo, Ondigi aliomba wakazi kukumbatia kilimo cha kisasa kwa kufanya upanzi wao ndani ya vivungulio (Green houses) ili kutoendelea kupata hasara kubwa.

“Tena ikiwa tunahitaji kuzuia hasara zaidi sharti tuanze kufanya kilimo kwa njia ya kisasa ili kunogesha sekta hii ya kilimo,” aliongeza Ondigi