Idara ya Afya katika Kaunti ya Mombasa itazindua ambulensi za kuwasafirisha wagonjwa zilizo na muundo wa tuktuk, zitakazoweza kupenya hadi vijijini ili kukabiliana na dharura zozote za kiafya katika Kaunti hiyo.
Mkuu wa Idara ya Afya katika Kaunti ya Mombasa Mohammed Abdi amesema hatua hiyo itawawezesha wanawake wajawazito, watoto na wakaazi wengine watakaokumbwa na matatizo ya kiafya kusafirishwa hadi katika zahanati zilizo karibu ili wapate huduma za dharura.
Akizungumza katika eneo la Mikindani baada ya kutembelea zahanati za eneo hilo siku ya Alhamisi, Abdi alisema kwamba ni lazima sekta ya afya katika Kaunti ya Mombasa ipewe kipau mbele kwa lengo la kuhakikisha kwamba visa vya dhrura vya kiafya vinavyowakumba wakaazi katika kaunti hiyo vinakabiliwa.
"Tunapanga mikakati mwafaka ya kuhakikisha kuwa zahanati zetu zinapata magari maalum ya kusafirisha wagonjwa wakati wa dhararu ili kuhakikisha kuwa huduma bora za afya zinatolewa kwa wakaazi wa Mombasa,” alisema Abdi.
Wakati huo huo, mkuu huyo wa Idara alidokeza kwamba Serikali ya kaunti hiyo ikishirikiana na Shirika lisilokuwa la Kiserikali kutoka nchini Marekani la USAID litazindua hazina ya shilingi milioni 20, itakayowafadhili wanafunzi watakaojiunga na taaluma ya afya ili wahudumu katika hospitali na zahanati za kaunti hiyo.
Serikali ya kaunti ilizindua ujenzi wa zahanati na wadi za kujifungua katika maeneo ya Likoni, Mtongwe na Changamwe.