Serikali ya Kaunti ya Kiambu kwa ushirikiano na shirika la kufadhili miradi ya maendeleo duniani IFC, inapanga kuweka mfumo wa kuwawezesha wanaoendesha miradi ya ujenzi kupata kibali kwa chini ya siku saba.

Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Mfumo huo kwa jina 'e-development system' utawezesha kila kanuni kuhusu ujenzi kutimizwa na wanaopanga miradi hiyo kwa urahisi na bila mapendeleo.

Akizungumza siku ya Jumatatu wakati kampuni ya uwekezaji ya Cytonn Investments Ltd ilikuwa ikizindua mradi wa ujenzi wa nyumba zaidi ya 400 za kupanga katika eneo la Ruaka, Gavana wa Kaunti ya Kiambu William Kabogo alisema kuwa atakayekuwa wa kwanza kuwasilisha ombi la kupewa kibali na serikali ya kaunti, ndiye atakuwa wa kwanza kushughulikiwa.

"Hatua hii imesababishwa na haja ya kuhakikisha kuwa majengo ya kaunti ni ya viwango vya hali ya juu na kuwa yamejengwa mahali halali na kwa njia halali,” alisema Kabogo.

Aliongeza, “Isitoshe, kwa vile tunataka kaunti hii iwe mbele zaidi kimaendeleo, mfumo huo utawasaidia wenye miradi ya ujenzi kumaliza shughuli za kutafuta kibali kwa muda mfupi."