Wizara ya Afya katika kaunti ya Kisii,imeweka mikakati kabambe ya kupambana  na ongezeko la virusi vya ugonjwa wa ukimwi  katika kaunti hiyo.

Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Akiongea jana katika jengo la kitamaduni mjini kisii wakati wa hafla iliyojumuisha wakazi na viongozi wa Kaunti hiyo ili kujadiliana  na changamoto  zinazowakumba wakazi, Daktari Mkuu wa afya katika kaunti ya Kisii Geofrey Ontomu, alisema kutokana  na ripoti aliyonayo ni kuwa kuna ongezeko la asilimia 2.2 ikilinganishwa na hapo mbeleni wakati sekta ya afya ilifanya juhudi za kuhakikisha kuwa ongezeko hilo limepungua.

Kulingana na Daktari Ontomu, serikali ya kaunti ikishirikiana na sekta ya afya inaendelea kuweka mikakati kabambe ya kuhakikisha kuwa ugonjwa huo hatari umepungua pakubwa.

Hapo mbeleni walikuwa wamehakikisha  kuwa  asilimia hiyo imepungua hadi 6.8% lakini kwa sasa asilimia hiyo imeongezeka hadi 9% kwa hivyo viwango hivyo vimeongezeka kwa asilimia 2.2 jambo Ontomu amesema kuwa litashughulikiwa kwa haraka kabla ya viwango hivyo vya ugonjwa huo kuongezeka zaidi.

Kwa upande wake gavana wa kaunti ya Kisii amewaomba wakazi wote kujiepusha na mambo yatakayochangia kuathiriwa kwa ugonjwa huo huku akisema serikali yake itahakikisha kuwa wameweka mikakati kabambe ya kupambana na ugonjwa huo.

Aidha amewaomba  wanafunzi wa vyuo vikuu katika kaunti ya Kisii kujua na kufahamu hatari za ugonjwa huo bila kuchukulia janga au ugonjwa huo kama  jambo la kawaida na kuwaomba kujilinda kwa kuwa wao ndio kizazi cha kesho.

"Watu wanastahili kujikinga kutokana na vitendo mbalimbali ambavyo vinaweza sababisha  kuadhiriwa na ugonjwa huo hatari," alihoji Ongwae.

Kwa upande mwingine Ongwae alikashifu baadhi ya wakazi wanao sema kuwa hospitali ya rufaa na mafunzo ya Kisii kuwa haina vifaa vya kutosha  huku akisema kuwa hospitali hiyo ina vifaa vya kutosha na huduma ya afya  inaendelea kwa njia shwari.