Siku chache tu baada ya kampuni ya kutengeneza Soda ya Coca-Cola kuonyesha nia ya kusafisha Mto wa Nyakumisaro, Kaunti ya Kisii sasa imeahidi kushughulikia mto huo kabla ya mwaka huu kuisha.
Akiongea hii leo katika mji wa Kisii, Gavana wa Kaunti hiyo James Ongwae amethibitisha kuwa Serikali ya Kaunti hiyo kupitia Wizara ya Maji na Mazingira imeweka utaratibu wa kuona kwamba mto huo, ambao maji yake hutumika na wakaazi wengi wa mji huo, umesafishwa na miti kupandwa kando yake ili kuulinda kutokana na uchafu wa kimazingira.
“Mto wa Nyakumisaro ndio wa kipekee kutusambazia maji katika Kaunti yetu na nawaomba watu wote wanaokaa karibu na mto huo kutusaidia kudumisha usafi katika mto huo huku tukipanga usafi wa mto huo,” alisema Gavana Ongwae huku akiwatahadharisha watumizi wa mto huo dhidi ya kuchafua mto huo.
Mto huo ni wa kipekee ambao umepita kati ya mji wa Kisii na wakazi, viwanda na watengenezaji haswa wa magari humwaga uchafu humo bila kuwasahau vijana wa kurandaranda ambao ukoga katika mto huo.
Kibarua kitabaki kwa Serikali ya kaunti hiyo ya kuona wanakomesha wenye viwanda hao ambao wamechangia pakubwa kuchafua mto huo.