Kaunti ya Kisii imejitolea kupigana na maradhi ya saratani na wito umetolewa kwa wakaazi wote kujitokeza tarehe moja mwezi Juni ili kupata mstibabu ya bure katika Hospitali ya Rufaa ya Kisii Level Six.
Akiongea siku ya Jumatano jioni na Waandishi wa Habari katika ofisi yake, Anayesimamia Wiziri wa Afya katika Kaunti ya Kisii Sarah Omache alisema kuwa Serikali ya Kaunti ya Kisii kwa ushirikiano na Hospitali moja kutoka India kwa jina BLK watatoa matibabu ya bure ya saratani katika Hospitali ya Rufaa ya Kisii Level Six.
Omache alisema kuwa hatua hiyo iliafikiwa baada ya Maafisa kutoka Kaunti hiyo kutembelea nchi ya India na kuteua hospitali hiyo ya BLK ambayo Omache alisema kuwa maarufu kwa kutoa tiba ya ugonjwa wa saratani.
"Nawaomba wakaazi wote Kisii kuja tarehe moja katika ili kupimwa na kupata matibabu iwapo watapatikana na ugonjwa huo. Matibabu yatakuwa ya bure,” alisema Omache.
Huu ni mradi wa tatu wa kutoa matibabu ya saratani katika Kaunti ya Kisii tangu mwaka huu uanze na juhudi hizo zimeshuhudia wananchi wengi kutoka Kisii wakikumbatia matibabu hayo.