Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Serikali ya Kaunti ya Kisii imetangaza kuchukua usimamimizi wa nyumba ya hifadhi ya mayatima ya Kisii iliyokuwa inasimamiwa na shirika la Maslahi ya Watoto Nchini Kenya, tawi la Kisii.

Nyumba hiyo, ambayo ilianzishwa rasmi mnamo mwaka 1969, ilikabidhiwa shirika hilo la kuwatunza mayatima na watoto wengine walioathirika na changamoto za maisha katika mwaka wa 1974.

Akizungumza na wana habari katika hafla iliyoandaliwa kutangaza hatua hiyo ya serikali ya kaunti, Pius Abuki ambaye ni mkurugenzi wa kamati teule ya bunge iliyobuniwa kutatua swala la ardhi ya umma Kaunti ya Kisii, alielezea kwamba shirika hilo lilikuwa limekabidhiwa nyumba hiyo kwa minajili ya kuwatunza na kuwatetea mayatima na watoto wasiokuwa na makao lakini baada ya muda mfupi baadhi ya wakurugenzi wake walijiundia stakabadhi bandia za kuthibitisha kwamba wao ndio wenye hati miliki za kipande cha ardhi ambacho kimejengwa jengo hilo.

“Jambo tunalolielewa na kulifahamu kama wanakamati ni kwamba shirika hilo lilipewa nafasi ya muda ya kuwashughulikia mayatima na watoto walio taabani lakini lile ambalo hatujalielewa hadi sasa ni hali ipi iliyopelekea walipa kodi kugeuka na kuwa wenye hati miliki ya ardhi ya umma," alisema Abuki.

Abuki alisema kwamba kamati ya kutatua unyakuzi wa ardhi ya umma alidokezea kwamba serikali ya kaunti ina mchakato maalum wa kujipanga upya hasa katika swala tata la ardhi iliyonyakuliwa na kusema kwamba hatua hiyo ni mojawapo ya mikakati yake ya kuhakikisha kwamba mpango huo unatekelezwa kikamilifu.

“Serikali ya kaunti ya Kisii inanuia kutenga ardhi maalum kwa mpango wa kuwarekebisha waathiriwa wa vileo na mihadrati katika kaunti hii na kuitwaa ardhi hii ni hatua muhimu ya kufanikisha mpango huo," alieleza Abuka.

Abuka aliendelea kusema kuwa serikali ya Kisii imefanya majadilano na Shirika la Kupambana na Vileo na Mihadarati NACADA, na shirika hilo limesema kuwa linataka kujenga kituo cha kurekebisha waathiriwa wa vileo na mihadharati katika eneo hilo.

Kwa sasa serikali ya Kisii imetenga jumla ya ekari nne kwa shughuli hiyo na ardhi hiyo ni sehemu za kituo hicho.

 “Ardhi hii ni rasilmali halali ya serikali ya kaunti na yanayojiri hapa siku ya leo ni urejeshi wa mali chini ya utawala au miliki ya wanaostahili," alisisitiza mbunge huyo.