Serikali ya kaunti ya Kisii imepata mkopo wa shilling billioni mbili za kuanzisha kituo cha kupima na kutibu ugonjwa wa saratani katika hospitali ya Rufaa ya Kisii.

Share news tips with us here at Hivisasa

Hii ni baada ya serikali hiyo kutia sahihi ya maelewano siku ya Jumatano katika jengo la Crowns plaza jijini Nairobi kati ya waziri wa pesa nchini Henry Rotich, benki ya Arab Bank Economic Development For Africa na gavana wa kaunti ya Kisii James Ongwae.

“Sasa nitawaamrisha maafisa wangu kuanzisha ujenzi wa kituo hicho mara moja ili ukamilike haraka na watu waaze kuhudumiwa mara moja,”alisema gavana James Ongwae.

Aliongezea: “Tumetia sahihi na benki ya Arab Bank Economic Development For Africa ya shillingi billioni moja na pesa hizo zingine tutazipata kutoka kwa Saud Fund. Pesa hizo zitatumika kujenga kituo hicho katika hospitali ya rufaa ya Kisii.”

Ongwae alisema kituo hicho kitawasaidia watu wengi maana ndicho kituo cha kwanza kujengwa katika mkoa wa Nyanza na katika South Rift.

Aidha, utafiti unaonyesha kuwa ugonjwa wa saratani umewaathiri watu wengi wa jamii ya Kisii lakini kwa sasa watakuwa wakipata huduma katika hospitali ya rufaa ya Kisii.

Hafla hiyo ilihudhuriwa na waziri wa afya katika kaunti ya Kisii Sarah Omache, waziri wa Fedha na maafisa wengine wa serikali ya Kisii.