Kaunti ya Kisii imeibuka na ushindi katika mashindano ya riadha kwenye ubingwa wa shule za msingi ambayo yalianza siku ya Jumapili na kukamilika leo Jumatatu.
Mashindano hayo ambayo yaliandaliwa kwenye uga wa chuo cha Kisii, yalijumuisha kaunti sita kutoka mkoa wa Nyanza, yaliweza kushuhudia kuteuliwa timu ambayo itawakilisha eneo la Ziwa Kuu (Lake Region) katika mashindano ya Kitaifa ya riadha ya shule za msingi ambayo yatafanyika katika uga wa michezo wa Gusii Green.
Akiongea na huyu mwandishi, mkurugenzi wa elimu katika kaunti ya Kisii ambaye alikuwa mmoja wa maafisa waandalizi wa michezo hiyo, Bwa Richard Chepkawai alisema kuwa wanalenga kuimarisha michezo yote ya riadha katika kaunti ya Kisii na kudokeza kuwa watahakikisha kuwa wanaboresha matokeo yao zaidi ya jinsi wafanya leo.
“Tutashirikiana na maafisa husika wote kutoka kwenye kaunti ya Kisii kuona kwamba tunafanya vizuri zaidi na tutawaunga shule na wanafunzi ambao wameteuliwa leo kushiriki katika ubingwa wa kitaifa ambao utafanyika wiki kesho tarehe 12 kwenye uga wa Gusii au hapa Chuoni,” aliongeza Chepkawai.
Mashindano hayo yalijumuisha shule kutoka kaunti za maeneo Nyanza zikiwemo Migori, Homabay, Siaya, Kisumu, Nyamira pamoja na Kisii, ambao walikuwa wenyeji wa mashindano hayo ambapo vitengo mbali mbali vilishindaniwa kama vile mita elfu 10, mita 400 kupokezana vijiti miongoni mwa mashindano mengine.