Gavana wa kaunti ya Kisumu, Jack Ranguma, ametoa hakikisho kuwa serikali yake itaajiri waalimu 700 wa shule za chekechea hivi karibuni.

Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Akiongea afisini mwake siku ya Jumatatu wakati alipokutana na mkurugenzi mkuu wa shirika la Plan International Bi. Carol Sherman aliyemtembelea, gavana Ranguma alisema kaunti ya Kisumu inakabiliwa na uhaba wa waalimu wa chekechea.

Ranguma alisema kuwa shule nyingi za chechekea katika jimbo hilo zina miundo misingi duni lakini aliahidi kushughulikia changamoto hizo.

 “Lazima tuimarishe elimu ya checheckea katika jimbo letu. Hii itatusaidia kuwajengea watoto wetu misingi bora maishani,” akasema Ranguma.

Ranguma alikaribisha ushirikiano mpya kati ya Kaunti ya Kisumu na Plan International.

“Kama serikali ya kaunti ya Kisumu, tunakaribisha ushirikiano huu mpya na Plan International, kwa lengo la kuimarisha sekta ya elimu ya chekechea ambayo imesahaulika kwa muda mrefu,” akaongeza Ranguma.

Naye mkurugenzi mkuu wa Shirika la plan international Carol Sherman, alisema wameanza mchakato utakaochukua kipindi cha wiki moja, kuzuru kaunti za Kisumu, Homa Bay na Siaya ili kukagua miundo msingi kwenye shule za chechekea.

“Lengo kubwa la Plan International, ni kuhakikisha kuwa kila mtoto katika jamii amepewa fursa na nafasi ya kuafikia lengo lake maishani, kupitia kupata mazingira mwafaka ya elimu,” alisema Sherman.

Aliongeza kuwa miradi yao mingi inaegemea sekta ya elimu, akisisitiza kuwa wanachukulia kwa uzito mkubwa suala la elimu ya chekechea.