Wafuasi wa muungano wa Cord kaunti ya Mombasa wanatarajiwa kuungana na wenzao kote nchini siku hii leo kuandaa maandamano ya kushinikiza kuondoka afisini kwa maafisa wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka nchini IEBC.

Share news tips with us here at Hivisasa

Akizungumza kwenye hafla nje ya majengo ya bunge la kaunti ya Mombasa, Mwakilishi wa wanawake katika kaunti hiyo Bi Mishi Mboko amesema kuwa wakati umefika kwa mwenyekiti wa IEBC Isaak Hassan na makamishina wengine kuondoka afisini kwa kushindwa na kazi.

Kwa upande wake gavana wa Mombasa Hassan Joho amesema kuwa viongozi wa Jubilee wanalazimika kukubali mazungumzo ya upande wa upinzani kwa ajili ya kufanyiwa marekebisho tume ya IEBC akitaja kuwa hawana haja ya kuweka makamishina wao bali watakaokuwa waaminifu katika utendakazi.

Joho amesema kuwa serikali lazima isikilize maoni ya wakenya ambao wameonyesha kukosa imani na tume hiyo akisema kuwa kufanikishwa hilo kutajenga zaidi umoja na amani humu nchini huku nchi ikielekea kwenye uchaguzi mkuu mwaka ujao.

Haya yanajiri huku kinara wa Cord Raila Odinga akitoa wito kwa wafuasi wa muungano huo katika kaunti ya Nairobi na maeneo mengine nchini kujitokeza kwa wingi kila Jumatatu kwa ajili ya maandamano hayo ya kushinikiza kubanduka kwa makamishina wa IEBC.

Gavana Joho pia aliomba idara ya ulinzi kuhakikisha kuwa usalama umeimarishwa wakati wa zoezi hilo, kwani wanapanga kuwa na maandamano yaliyo sheheni amani katika mji wa Mombassa.