Serikali ya Kaunti ya Mombasa kupitia mkuu wa idara ya mifugo, uvuvi na kilimo Bw Antony Njaramba imethibitisha kuwa imeweka mipango kabambe ya kukabiliana na msimu wa kiangazi.

Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Akizungumza na wanahabari alipohudhuria kikao cha Tume ya kitaifa ya ardhi nchini NLC, katika taasisi ya Kenya School of Government, Njaramba alisema kuwa tayari wamegawa mbuzi wanoweza kustahamili ukame katika maeneo ya Likoni, Mwakirunge, Jomvu na Changamwe.

"Tumesaidia sehemu ambazo zilikuwa katika hatari ya kukabiliwa na kiangazi. Tumepeana mbuzi wanaoweza kustahamili ukame tukizingatia chakula kinachohitajika kwa mbuzi ni kichache kuliko mifugo kama ngo'mbe," alisema Njaramba.

Mbali na kilimo cha ufugaji, Njaramba alisema kuwa wanatoa mafunzo kwa wakulima kuhusu utumizi wa teknolojia katika upanzi wa mimea inayoweza kuhimili makali ya kiangazi.

“Tumewasaidia wakulima kutumia teknolojia katika kilimo ikiwa ni pamoja na kupanda baadhi ya mimea inayoweza kufanya vizuri wakati wa ukame ikiwemo mihogo, viazi tamu na matunda kama tikitimaji," alisema Njaramba.

Aidha, alisema kuwa chakula kinachozalishwa katika Kaunti ya Mombasa kinatosheleza mahitaji binafsi wala sio kuuzwa sokoni, swala ambalo limewapelekea kununua chakula kutoka masoko ya njee.

Kauli ya Njaramba inajiri huku Kaunti jirani ya Kilifi ikishuhudia baa la njaa, kutokana na uchache wa lishe unaendelea kusababishwa na makali ya kiangazi.