Kaunti ya Mombasa itakuwa mojawapo ya kaunti zilizo na miji ya hadhi ya kimataifa ifikapo mwaka wa 2035.
Akiongea wakati wa uzindizi wa mradi wa ruwaza ya mwaka wa 2035 ya Kaunti ya Mombasa iliyofanyika katika uwanjwa wa Mombasa Golf Club maeneo ya Mama ngina mjini Mombasa, Gavana wa Kaunti hiyo Hassan Ali Joho amesema kuwa Serikali yake imeweka mikakati kabambe ili kuhakikisha kuwa sekta zote za kiuchumi katika kaunti hiyo zinaimarishwa.
Joho aidha aliongeza kuwa miundo misingi katika kaunti hiyo itaboreshwa ili kuwavutia watalii pamoja na wawekezaji kutoka pembe zote za ulimwengu.
“Mradi huu tuliyozindua utachangia uboreshaji wa maswala ya kiuchumi na uwekezaji mkubwa katika kaunti ya Mombasa,” alisema Joho.
Ruwaza hiyo ya mwaka wa 2035 inalenga kuboresha kaunti ya Mombasa kimiundo msingi, mazingira, kitalii, nyumba za makazi miongoni mwa maswala mengine ya kiuchumi, kibiashara na kimaendeleo katika kaunti hiyo.
Hafla hiyo ilihudhuriwa na Gavana wa Kaunti ya Lamu Issa Timammy, Mbunge wa Mvita Abdulswamad Sharrif Nassir, Mbunge wa Kisauni Rashid Bedzimba miongoni mwa viongozi wengine.